OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzales, jana Jumamosi alifikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi yake hiyo, huku akitoa sababu kuu mbili nzito za kufikia uamuzi huo.

Barbara amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili tangu Novemba 17, 2020 akichukua nafasi ya Senzo Mbatha.

Katika taarifa ambayo aliitoa Barbara, alisema: “Leo (jana Jumamosi) nimeandika barua ya kujiuzulu nafasi yangu kama Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba kuanzia Januari mwakani. Nimetoa notisi ya mwezi mmoja ili nishiriki kuhakikisha kipindi kizuri cha mpito na makabidhiano na menejimenti mpya.

“Ni jambo la fahari kwamba chini ya uongozi wangu kwa kushirikiana na Rais wa Heshima wa Klabu, Mwenyekiti wa Klabu na Bodi ya Wakurugenzi, wafanyakazi wenzangu, wachezaji na benchi la ufundi, wanachama, mashabiki  na wadau wengine klabu ilipata mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja.

“Nimechukua uamuzi huu kwa sababu kubwa mbili, mosi kutoa nafasi kwa Bodi Mpya ya Wakurugenzi itakayochaguliwa kwenye uchaguzi ujao kuchagua CEO mpya atakayeendana na dira yao. Pili kujipa nafasi ya kutimiza ndoto na fursa nyingine kwingineko. Nachukua nafasi hii kuwashukuru wote na Simba itabaki moyoni mwangu na nitaendelea kuwa Mwanasimba.”

Januari 2023, Simba inatarajiwa kufanya uchaguzi wa nafasi sita ikiwemo kumpata mwenyekiti na wajumbe.

Cc @irundetz

#irundereports

Post a Comment

 
Top