Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba Akitoa Maelekezo kwa Viongozi Wilayani Manyoni Kuhusu Upandaji Miti.

WAKATI Mkoa wa Singida ukijiandaa na maadhimisho ya Siku yake ambapo unatimiza Miaka 60 imeanzishwa kampeni ya upandaji miti ambapo jumla ya miti 254,880 imepandwa tokea zoezi hilo lilipoanza tarehe 07 January 2023.

Zoezi hilo linatekelezwa kila siku ya Jumamosi ambapo kwa wiki hii Wilaya mbili za Ikungi na Manyoni zilipanda idadi hiyo ya miti mbapo Ikungi imepandwa miti 54,000 na Manyoni miti 200,880 toka kuanza kwa kampeni.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewapongeza wananchi wa Wilaya hizo na kuwataka kuzilinda na kuitunza miti hiyo ili iweze kukua.

Akiongea na wananchi wa Wilaya hizo leo wakati wa zoezi la upandaji miti lililoanzia katika mpaka wa Manispaa ya Singida na Ikungi mpaka  Kintiku mpakani mwa Dodoma na Singida ambapo RC Serukamba amesema lengo la Mkoa ni kupanda miti Milioni tatu kwa Mkoa mzimai (3,000,000) kwa mwaka 2023.

RC Serukamba ameeleza kwamba miti hiyo inapandwa katika maeneo ya kingo za Barabara kufuata bikoni zake, mashuleni Hospitalini, vyanzo vya maji, majumbani na kwenye nyumba za ibada. 

Aidha Serukamba ameagiza Wakuu wa shule kupitia Maafisa Tarafa na kata kuhakikisha miche inapatikana mashuleni ambapo kila Mwanafunzi atapatiwa miti minne wakapande nyumbani kwao.

Hata hivyo RC ametoa maagizo kwa wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani kuhakikisha wanatunga Sheria kali zitakazo wafanya wafugaji kuwa makini na mifugo yao sambamba na kuweka faini kubwa kwa atakaye sababisha mfugo kula miti hiyo.

Serukamba ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Ikungi kuhakikisha wananchi wa Ikungi wanapunguza tabia ya ukataji miti hovyo na uchomaji wa mkaa kwakuwa imeonekana eneo hilo ndilo athirika zaidi.

Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa huo ameahidi kuwakutanisha Wakuu wa Wilaya wote na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayojishughulisha na uboreshaji wa Miche ili waweze kuisaidia halmashauri ambazo zina changamoto hiyo.

Kwa upande wake DC wa Ikungi Jerry Muro amesema wameshaweka mkakati kupitia Maafisa Tarafa na kata kuhakikisha kuwa wanapanda miti Milioni moja na laki tano kwa Wilaya nzima.

Amesema Mpango huo utakamilika kwa kuanzisha vitalu vya miti kila kata ambapo itakuwa rahisi kuisambaza kwa wananchi na kuzisimamia kikamilifu.

Jerry Muro ameeleza changamoto ambayo inaweza kutokea ni upungufu wa miche ambapo amemuomba Mkuu wa Mkoa huo kuharakishwa kuwakutanisha na wadau wanaozalisha miti ili zoezi lisikwame.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro Akimwagilia Maji Mti ambao Ameupanda Mpakani kwa Wilaya ya yake na Wilaya ya Singida.

Naye DC wa Manyoni Rahabu Mwagisa amesema wameweza kupanda miti  200,880 kwa kushirikiana na Taasisi ya Wakala wa misitu Nchini (TFS) na muitikio mzuri wa wananchi.


Post a Comment

 
Top