Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba Akizungumza Mara Baada ya Kusikiliza Kero.

 Maafisa wa ardhi, Watendaji wa Vijiji na Kata Wilayani Mkalama wametakiwa kuacha vitendo vinavyosababisha migogoro ya ardhi ambayo imetajwa kama chanzo cha umaskini kwa wananchi wa Wilaya ya Mkalama.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba alipokutana na wananchi wa Wilaya hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo ambapo walimueleza kero nyingi zikiwemo za  ardhi.

RC amewataka Maafisa ardhi, na Watendaji wa Vijiji na Kata kuacha kushiriki vitendo vya uuzaji wa ardhi ambazo tayari zinaumiliki wa watu wengine na badala yake wajikite kuwashauri wananchi kuhusiana na mambo ya ardhi.

Aidha akiwa katika kikao hicho RC Serukamba alipokea kero 49 ambapo 43 zilikuwa zikihusisha migogoro ya mashamba na viwanja baina ya mtu na mtu au mtu na Serikali ya kijiji ambapo Maafisa ardhi na Watendaji wa kata na vijiji walikiri kuifahamu lakini hawakuweza kuitatua kwa namna yeyote ile.

RC Serukamba amesema wananchi wanategemea mashamba na viwanja hivyo kufanya maendeleo ya kiuchumi lakini kupitia utendaji usioridhisha wa viongozi hao wananchi wamekuwa wakipoteza mashamba yao na kusababishiwa umaskini.

"Maafisa ardhi, Watendaji wa kata na vijiji msiwe chanzo cha umaskini wa wananchi, watu wanataka kulima wengine wanataka kufanya maendeleo lakini mnawakwamisha mnaposhindwa kuwatatulia shida zao" Serukamba.

Kufuatia hali hiyo RC Serukamba amewagiza Watumishi kutekeleza wajibu wao kikamilifu ambapo amesema kwa kufanya hivyo kutapunguza kero za wananchi.

"Kila Mtumishi ajitafakari kwamba kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa amefanya nini katika kutekeleza wajibu wake? Kwakuwa wapo watu wanakuwepo kazini kila siku lakini hakuna anachokifanya" Serukamba

Hata hivyo RC Serukamba anaendelea na ziara yake ya kusikiza kero za Wananchi na siku ya kesho itakuwa zamu ya wananchi wa Wilaya ya Ikungi.


Post a Comment

 
Top