Mkuu wa Mkuu wa Singida Peter Serukamba Akishuhudia Kibao cha Jiwe la Msingi katika Ujenzi Ofisi ya Madereva.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameweka rasmi jiwe la msingi katika ujenzi wa Ofisi ya madereva Mkoani hapo  linalotarajiwa kugharimu zaidi ya Tsh. Milioni 79.6.

Akizungumza na Watumishi baada ya kuweka jiwe hilo RC Serukamba amempongeza Katibu Tawala wa Mkoa huo Dorothy Mwaluko kwa kuleta wazo la kuwajengea Ofisi madereva ili waweze kujikinga na mvua jua na baridi jambo ambalo ameeleza kwamba litaleta ufanisi katika kazi yao.

RC amesema maamuzi hayo ni ya kijasiri kwakuwa Ofisi nyingi za Serikali hazina Ofisi maalum  za madereva hivyo akawataka madereva hao kutunza Ofisi hiyo na kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Katika hatua nyingine ameupongeza mpango wa kuwa na sare maalumu inayovaliwa siku ya Ijumaa huku akiueleza  kwamba inaonesha umoja katika kazi.

Amesema umoja huo utumike katika ufanyaji kazi kwa umahiri juhudi na maarifa na kila Mtumishi ahakikishe kwa nafasi yake anatatua changamoto za wananchi.

"Utanashati huu nilio uona usiwe wa siku ya Ijumaa pekee bali tujitahidi siku zote tupendeze, mtu mtanashati hata kazi zake anazifanya vizuri" Serukamba.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Dorothy Mwaluko amemueleza RC Serukamba kwamba ujenzi wa ofisi hiyo ni sehemu ya majengo mbalimbali yanayoendelea kujengwa na ofisi hiyo yakihusisha nyumba za Maafisa Tarafa ambazo nazo atakaribishwa kuzizindua siku chache zijazo.

Aidha akiongea na Watumishi hao Mwaluko amewataka  kuongeza juhudi katika kufanya kazi na kuacha mazoea katika kazi  ili kuwasaidia wananchi wa Singida huku akikemea swala la utoro kazini.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Mwl Dorothy Mwaluko Akizungumza na Watumishi Katika Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ofisi za Madereva.

Awali akitoa taarifa ya awali Mhandisi wa Mkoa Domicianus Kirina amesema ujenzi wa ofisi hiyo ulianza tarehe 19 Desemba, 2022 ambapo inategemewa  kukamilika tarehe 1 Machi, 2023.

Ameleeza kwamba katika kufanikisha zoezi hilo ziliundwa kamati nne ambazo ni kamati ya manunuzi, mapokezi, ulinzi na kamati ya ufuatiliaji.

Mhandisi Domicianus  amesema fedha ambazo zimekwisha tumika zilikuwa ni Tsh. Milioni 56.04 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali na malipo ya fundi.


Post a Comment

 
Top