Katibu Tawala Mkoa wa Singida amekabidhi pampu 13 za umwagiliaji zinazotumia nishati ya jua kwa vikundi 13 vya vijana kutoka Halmashauri ya Manyoni, Itigi, Mkalama, Singida, Manispaa na Iramba zenye thamani ya Sh.Milioni 23.4.

Akiongea na vijana hao katika ukumbi wa Ofisi za Shirika lisilo la Kiserikali la SEMA Mkoani hapo amesema mashine hizo zitawasidia kuongeza kipato katika shughuli za kilimo cha bustani na kuwataka wazitunze ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Aidha Katibu Tawala huyo ametoa wito kwa vijana kuacha kulalamika kwamba hakuna ajira na badala yake wajitume kufanya kazi za kilimo na ufugaji kwa kuwa bidhaa zitokanazo na shughuli hizo zina soko kubwa ndani ya Mkoa na nje.

Aidha Katibu Tawala amelishukuru Shirika la NSV (Nedhalend Development Organization) kupitia Mradi wake wa OYE (Opportunities for youth Employment) kwa msaada wa mashine hizo ambazo zimegharimu kiasi cha Milioni 1.8 kwa kila moja ambapo shirika limechangia asilimia 68 na Kampuni iliyotengeneza ikachangia asilimia 15 wakati vikundi vikachangia asilimia 17 ambao inalipwa kwa miezi  16.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Usimamizi na Tathmini katika Mradi huo wa OYE  Belinda Masawe, amesema  mashine hizo hutumia nishati ya jua ambayo haitawaingizia gharama za uendeshaji Wanakikundi.

Hata hivyo Belinda ameendelea kufafanua kwamba mashine ina uwezo wa kumwagilia shamba lenye ukumbwa wa ekari mbili kwa msimu mmoja na ina uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka kumi (10) ukipata mafunzo.

Aidha ameeleza kwamba vikundi hivyo vimepewa muda wa miaka miwili (2) wa uangalizi na endapo zitaharibika kabla ya hapo vitarudishwa kwa muuzaji.

Akimalizia hotuba yake Belinda ameeleza kwamba mashine hizo zimetafutiwa ubora wake na kubainika kwamba ni nzuri kwa mazingira kwa kuwa hazitoi moshi wala mabaki ya mafuta ambayo yangechafua mazingira.

Awali akitoa maelezo ya ukaribisho Afisa vijana wa Mkoa wa Singida Fredrick Ndahani, ameeleza kwamba fursa za biashara katika Mkoa huo nikubwa kwa kuwa kuna miradi mingi imeanzishwa ikiwemo bomba la mafuta na miradi ya machimbo ya madini kwamba ni soko kubwa.

Ndahani ameendelea kueleza kwamba Serikali imeweka mazingira mazuri kwa vijana kuhakikisha kwamba wanajiajiri na wanapata mitaji kupitia mikopo ya Halmashauri ambapo kuna asilimia nne maaluma kwa ajili ya vijana.

Hata hivyo Ndahani aliwaeleza vijana hao kutumia fursa ya uwemo wa makao makuu ya Serikali Dodoma ambayo yapo karibu na Singida kupata masoko ya bidhaa zao huku akiwaasa kuboresha vifungashio.

Post a Comment

 
Top