Wahitimu wa Vyuo vikuu nchini wameaswa kutumia muda wao mwingi kujisomea vitabu mbalimbali vinavyoshabihiana na taaluma zao badala ya kutumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa elimu waliyopata inatakiwa kufanyiwa kazi na kuongeza marifa mapya kila mara.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa fedha na mipango Dkt. Mwigulu Nchemba katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba wakati wa maafali ya 20  yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Chuo cha Uhasibu (TIA) Mkoani hapo.

Akisoma hotuba hiyo Serukamba, amewataka wanachuo hao kutumia muda mwingi kusoma vitabu na kujikumbusha mambo waliojifunza ili kuongeza umahiri katika kazi za uhasibu badala ya kutumia muda wao kwenye mitandao ya  kijamii.

Aidha amewataka wahitimu hao kufanya kazi kwa haki, juhudi kubwa ubunifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilifu kwa kuwa Taifa linategemea kwa kiasi kikubwa mchango wao.

"Elimu mlizopata zitadumu kwa miaka mitano tu endapo hamtaweza kuzifanyia kazi pamoja na kusoma vitabu hasa kipindi hiki ambacho dunia inatumia teknolojia kuendesha mambo, niwakumbushe kwamba ili upate mafanikio ni lazima ufanye kazi kwa bidii uaminifu na kwa weledi" Alisema Serukamba.

Hata hivyo RC Serukamba ameipongeza bodi ya ushauri ya taasisi ya chuo cha Uhasibu kwa kuboresha mitaala ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupambana na mahitaji ya soko.

Hata hivyo RC Serukamba alimalizia hotuba yake kwa kuishukuru Taasisi hiyo ya Uhasibu kwa ushirikiano mkubwa na Serikali huku akibainisha kwamba watumishi wengi wa Serikali wanapata mafunzo kazini kupitia chuo hicho.

Awali akitoa hotuba yake Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya chuo hicho Wakili Saidi Musendo Chiguma, amesema Taasisi inatoa elimu inayoendana na mahitaji ya soko hivyo kusababisha chuo hicho kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi zaidi ya elifu 25.

Aidha ametoa ushauri kwa wahitimu hao kutumia elimu waliyopata kuiletea nchi maendeleo ya kiuchumi huku akiwataka wasiishie hapo badala yake waendelee kuongeza viwango vya elimu.

"Elimu ni kama kiumbe hai inatakiwa itumike na iwe inahuishwa mara kwa mara vinginevyo inakufaa" alisema Musendo.

Aidha ameshauri Serikali kuboresha sera ya elimu ili iweze kubadilisha maisha ya watu na iweze kuuzika kuirahisi kwenye soko la ajira.

Awali Musendo alifafanua kwamba jumla ya wahitimu katika chuo hicho kwa mwaka huu ni 3666 ambapo kati yao 1789 ni wanawake na 1868 ni wanaume katika ngazi ya Astashahada na Shahada, maafali hayo yamehusisha tawi la Singida, Mwanza na Kigoma.

Post a Comment

 
Top